MWAKA 2000 KATIKA
KALENDA YA MUNGU
Kama vile
kunavyokuwako na mwisho wa dakika, saa, siku, wiki, mwezi, mwaka, karne,
milenia au “millennium”, ndivyo kutakavyokuwako pia na “mwisho wa dunia” na
“siku za mwisho”. Chenye mwanzo, hakikosi kuwa na mwisho. Biblia inaeleza juu
ya siku za mwisho (1 TIMOTHEO 4:1), mwisho wa dunia (MATHAYO 24:3), n.k. Sasa
basi, maandiko matakatifu yanatuonyesha kwamba tunapaswa kujiangalia, ili siku
ya mwisho isitujie ghafla; kama mtego unasavyo ( LUKA 21:34-35 ). Ndiyo maana
leo, tunajifunza somo,”MWAKA 2000 KATIKA
KALENDA YA MUNGU”. Tutajifunza somo hili, kwa
kulitafakari katika vipengele vine:-
( 1 ). MWAKA 2000
KATIKA KALENDA YA MUNGU
( 2 ). KUNYAKULIWA
KWA WATAKATIFU
( 3 ). DHIKI KUBWA
AMBAYO HAIJAWAHI KUTOKEA TANGU
KUUMBWA KWA ULIMWENGU
( 4 ). JINSI YA
KUFANYA ILI KUNYAKULIWA
( 1 ). MWAKA 2000
KATIKA KALENDA YA MUNGU
Katika Kalenda ya Mungu, inayothibitishwa na Historia
ya Biblia, tunapomaliza mwaka huu wa
2000, inakuwa imetimia miaka 6000 tangu
Adamu, mtu wa kwanza alipoumbwa na kuishi duniani. Kuanzia wakati wa kuumbwa
Adamu mpaka wakati wa kuzaliwa Ibrahimu, ni miaka 2000. Kuanzia wakati wa
kuzaliwa Ibrahimu mpaka wakati wa kuzaliwa Yesu Kristo, ni miaka 2000. Wana
historia wakubwa wa karne ya kwanza hadi ya nne kama mwanahistoria mkubwa
JEROME aliyeishi katika miaka ya mwisho ya karne ya 4, kunako mwaka wa 392.
B.K; alihifadhi historia kubwa ya vizazi vya wanadamu. Sasa basi, katika
unabii, miaka 1000, ni sawa na siku moja ( 2PETRO 3:8 ). Hivyo inapotimia miaka
6000 ,maana yake, zinakuwa zimetimia siku sita, na tunapoanza sasa milenia au
millennium nyingine au miaka 1000 mingine, maana yake ni kwamba, tunaanza siku
ya saba. Katika kalenda ya Mungu, miaka hii 2000 baada ya Yesu Kristo
inayotimiza siku sita tangu Adamu inaitwa siku za mwisho.
Miaka ipatayo 34 baada ya kuzaliwa Kristo, ndipo ilipotimia
siku ya pentekoste, ambayo wanafunzi wa Yesu walipokea nguvu ya Roho
Mtakatifu(LUKA 3:23, MATENDO 1:1-14; 2:1-4). Ujazo huu wa Roho Mtakatifu,
uliwafanya watu wengi kufikiri ni kulewa mvinyo mpya, na Petro aliposimama
kufafanua, alisema kwamba jambo hilo limetokea katika siku za mwisho sawasawa
na unabii wa Nabii Yoeli(MATENDO 2:5-18). Kumbe basi milenia mbili baada ya
Kristo inatimiza siku ya sita inayofayofanya siku za mwisho. Ni kama siku ya
ijumaa, mwisho wa wiki. Na siku ya saba, ni kama jumamosi katika wiki. Zamani
hizo za unabii wa Nabii Yoeli, siku ya saba, yaani jumamosi katika wiki ilikuwa
sabato.
( 2 ). KUNYAKULIWA KWA WATAKATIFU
Milenia ya saba tayari inatangazwa kuanza mwanzo wa mwaka
huu tarehe 1 january 2000. Maana yake ni kwamba tayari tumeanza siku ya saba.
Ni mapema alfajiri siku ya saba katika unabii.Siku hii ya saba kama
tulivyokwisha kujifunza, Yesu atakuja mawinguni, na kwa namna ya sumaku kuvuta
chuma, atawavuta au kuwanyakua watakatifu walioko duniani ( 1WATHESALONIKE
4:13-17 ; ZABURI 16:3; 1WAKORINTHO 15:50-54 ). Kama ni usiku watakuwako wawili
kitandani mmoja aliyeishi mbali na dhambi atwaliwa, mmoja aliyelipuuza neno la
Mungu aachwa. Kama -ni mchana, wawili watakuweko kondeni (shambani ), mmoja
atwaliwa, mwingine aachwa,(MATHAYO
24:40-41) .Kunyakuliwa kwa kanisa hasa kutakuwa siku ipi, tarehe ipi, mwezi
upi, au mwaka upi? Biblia haitaji tarehe halisi, tunachojua tu ni siku ya saba
na dalili zake zote tayari. Yesu anakuja ghafla kama mwivi wa namna
iliyozoeleka, asivyotoa taarifa ya kuja kuiba. Hata hivyo wengi wasiojua kwamba
tayari siku ya saba imeanza, watajikuta hawajitayarisha ( MATHAYO 24:3-14,
36-41 ).
( 3 ). DHIKI KUBWA
AMBAYO HAIJAWAHI KUTOKEA TANGU KUUMBWA
KWA ULIMWENGU
Baada tu ya kunyakuliwa watakatiifu, hapa duniani kwa wale
wenye dhambi ambao hawakutaka kutubu dhambi zao, na kuziacha ili waokolewe
kutoka katika dhiki hiyo, watakuwa katika dhiki hiyo, watakuwa katika dhiki
kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu kuumbwa kwa ulimwengu ( MATHAYO 24:21 ).
Dhiki hii itakuwa ya miaka saba na itakuwa ya kutisha. Watu watatamani kufa,
lakini mauti itawakimbia (UFUNUO 9:1-10 ; 6:15-17; 16:1-21). Kama ilivyokuwa
siku za Nuhu na wakati wa Sodoma na Gomora, Mungu hawaadhibu waliowake. Wenye
haki hutengwa pembeni kabla ya wasiohaki kuteswa kwa ghadhabu ya Mungu. Kwa
sababu hiyo, watu waliojitenga na dhambi, wataokoka kutoka katika dhiki kubwa.
Nuhu na jamii yake wenye haki waliondolewa na kuwekwa safinani kabla ya ghalika
kuja. Luthu na jamaa yake wenye haki walitengwa na wenye dhambi kabla ya Sodoma
na Gomora kuteketezwa ( MWANZO 18:20-33; 19:1-24; MATHAYO 24:37-39; LUKA 17:26,
28-30 ).
( 4 ). JINSI YA KUFANYA ILI KUNYAKULIWA.
Mungu wetu ni Mungu wa upendo, hapendi hata mmoja ateseke.
Moto wa milele na mateso yote ya jinsi hii hakuwekewa mwanadamu, bali Ibilisi
na malaika zake ( MATHAYO 25:41 ). Hata sasa Mungu anasubiri kwa upendo wake
ili tutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha na kuokolewa ( MITHALI 28:13;
WARUMI 2:4-5; 2PETRO 3:9 ).Kusamehewa dhambi zetu huambatana na kuokolewa
kutoka katika dhiki kubwa na hivyo kunyakuliwa na Bwana Yesu (LUKA 1:77 ). Yote
haya hufanyika kwa imani tu katika Yesu Kristo aliyejaribiwa sawasawa na sisi
katika mambo yote bila kutenda dhambi, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu si kwa uwezo
wetu wala kwa nguvu zetu ( ZEKARIA 4:6;
WAFILIPI 4:13; WAEBRANIA 4:14-16 ). Baada ya hapo kama watoto wachanga wa
kiroho tuzidi kujifunza neno ambalo ni maziwa yasiyoghoshiwa ( yasiyochanganywa
na maji ) ili tuukulie wokovu. Bila kuhudhuria ibada hizi kadri tunapopata
nafasi, ni rahisi tena kujikuta tumeanguka dhambini tena. Utakatifu hudumu kwa neno
( ZABURI 119:11; YOHANA 15:3 )..
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Ni sifa ipi
ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni
utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake
hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha
kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia
mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati
kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa
ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge,
mwenye dhambi. Sistahili kuingia
mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu
Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la
Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia
mbinguni. Ili uzidi kudumu katika
utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho
katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU
AKUBARIKI !!!
No comments:
Post a Comment