Ina maana gani kwamba mshahara wa dhambi ni mauti?

Warumi 6:23 inasema, "Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu." Katika msingi wake, dhambi ni uasi dhidi ya Mungu. Dhambi zetu hututenganisha na Mungu, Muumba na mwenye uzima. Yesu alisema, "Mimi ndimi njia na kweli na uzima" (Yohana 14: 6). Mungu anajulikana kama "MIMI NDIMI" mkuu. Uzima uu katika Mungu. Kwa hivyo, tunapofanya dhambi na kujitenganisha na Mungu, tunatengana na uzima wa kweli. Kwa hivyo, bila shaka, tunakumbana na mauti. Hoja tatu za ufafanuzi zinahitajika: Kwanza, dhambi hasa haisababishi kifo cha kimwili mara moja. Warumi 6 haituambii kwamba tunapofanya dhambi tutakufa kimwili. Badala yake, inarejelea kifo cha kiroho. Pili, wakati tunapookoka katika Kristo, tunaokolewa kutokana na hatima ya kifo cha kiroho na kuletwa katika hatima ya uzima wa kiroho. Paulo aliwaambia Warumi, "Zawadi ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu" (Warumi 6:23). Tatu, hata dhambi za waumini bila shaka zitasababisha aina ya "kifo" cha kiroho. Ingawa tumeokolewa kutokana na adhabu ya mwisho ya dhambi (kutengwa kwa milele na Mungu), hatuokolewa kutokana na matokeo ya asili ya uhusiano uliovunjika na Baba . Tunapofanya dhambi, tunapata dalili za kifo cha kiroho. Tunaweza kujihisi kuwa na hatia, kuwa wapungufu, kuchanganyikiwa, au kutokuwa na uhusiano na Mungu. Sisi hufanya kama waadilifu badala ya kuwa wenye haki. Dhambi zetu, hata kama waumini, huumiza moyo wa Mungu na uhuzunisha Roho Wake (Waefeso 4:30). Ingawa dhambi zetu haziachi uhusiano wetu na Yeye, huweka kizuizi kati yetu. Fikiria mtoto na mzazi. Wakati mtoto anapoasi, uhusiano na mzazi wake unafadhaika. Mzazi bado anampenda mtoto na bado ana nia bora kwa mtoto moyoni. Mtoto kamwe aachi kuwa bila mzazi. Hata hivyo, mtoto anaweza kupata matokeo fulani: kutoaminiwa, nidhamu, hisia ya hatia, na kadhalika. Bila shaka hatimaye uhusiano hurejeshwa ila kawaida pigo huja kwanza. Hivyo ni pamoja nasi na Mungu. Tunapoasi dhidi ya utawala wa Mungu katika maisha yetu, tunaasi dhidi ya Uzima, na hivyo tunakumbana na mauti (kuvunjika kunaosababisha maumivu). Tunapomrudia Mungu, tunarudishwa tena kwenye ushirika wa kiroho na Mungu, hisia za lengo, haki, uhuru, nk. Baba mwenye furaha katika mfano wa Mwana mpotevu alisema vizuri zaidi: "Huyu mtoto wangu alikuwa amekufa na yu hai tena "(Luka 15:24).

HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU

 

HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU

 

   Leo, tunaendelea kujifunza Sura ya 27 ya Kitabu cha MATHAYO, na tutaangalia MATHAYO 27: 50-66.  Katika mistari hii, tunajifunza juu ya kufa na kuzikwa kwa Yesu.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vitano:-

 

(1)  KUPAZA SAUTI KWA YESU NA KUITOA ROHO YAKE  (MST 50)

 

(2)  HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU (MST 51-54)

 

(3)  WANAWAKE KUMTUMIKIA   (MST 55-56)

 

(4)  KUZIKWA KWA YESU  (MST 57-61)

 

(5)  KULINDWA KWA KABURI  (MST 62-66)

 

(1)      KUPAZA SAUTI KWA YESU NA KUITOA ROHO YAKE   (MST 50)

 

Kulikuwa na giza juu ya nchi yote tangu saa sita hadi saa tisa mchana (MST 45).  Baada ya saa tisa mchana, yaani kati ya saa 9 -10 mchana, ndipo Yesu alipokata roho.  Kulikuwa na maana kamili juu ya kila jambo lililofanyika msalabani.  Saa tisa, ilikuwa ni saa ya kusali ya Wayahudi (MATENDO 3:1).  Saa nyingine za sala ilikuwa saa 3 asubuhi na saa 6 mchana.  Saa ya kusali saa 9, ndipo ulipokuwa wakati wa kutoa DHABIHU YA JIONI (DANIELI 9:21, 1 WAFALME 18:29, 36).  Saa hii ya jioni, ndipo Yesu alipokufa msalabani, na kutolewa kama DHABIHU YA JIONI kwa ajili yetu.  Wakati huu pia, ni ambapo mwanakondoo wa Pasaka alipochinjwa.  Yesu Kristo, alitolewa na kuchinjwa msalabani kama Pasaka wetu, mwanakondoo asiyekuwa na ila wala waa (1 WAKORINTHO 5:7; 1 PETRO 1:19).  Wakati wa kufa kwake Yesu, ALIPAZA SAUTI YAKE kudhihirisha nguvu alizokuwa nazo mpaka wakati wa kufa.  Hakika alijitoa MWENYEWE kufa kwa ajili yetu.  Kwa kawaida, watu wengi wanapokuwa wanakufa hawana nguvu ya kupaza sauti namna hii hasa baada ya mateso makubwa  namna hii.  Lakini, siyo hilo tu, alipaza sauti yake kwa nguvu, kama TARUMBETA zilizokuwa zikipigwa wakati wa kutoa dhabihu (HESABU 10:9-10).  Hakika, Kristo alikuwa dhabihu kwa Mungu, hatuna haja tena ya wanyama (WAEBRANIA 10:1-12; WAEFESO 5:2).

 

 

 

(2)      HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU  (MST 51-54)

 

Baada tu ya Yesu kuitoa roho yake, matukio kadha ya miujiza yalitokea, yaliyowafanya askari waliokuwa wanamlinda kusema “HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA WA MUNGU”.  Sasa, ebu tuyaangalie matukio haya na maana yake:-

 

    PAZIA LA HEKALU LIKAPASUKA VIPANDE VIWILI – Ni muhimu kukumbuka kwamba, ulikuwa wakati wa kusali na kutoa dhabihu ya jioni, katika hekalu.  Katika hekalu kulikuwa na Pazia la Hekalu, lenye urefu wa futi 60 kutoka darini hadi sakafuni.  Pazia hili liligawanya kati ya Patakatifu, na Patakatifu pa patakatifu, au mahali patakatifu sana (WAEBRANIA 9:1-3; KUTOKA 26:33).  Ilikuwa hakuna ruhusa ya mtu yeyote wa kawaida kuingia mahali patakatifu hata kuchungulia kwa dakika moja.  Akifanya hivyo, hukumu yake ni kifo (HESABU 4:17-20).  Mahali patakatifu waliingia makuhani peke yao.  Patakatifu pa patakatifu, aliingia Kuhani Mkuu peke yake, tena MARA MOJA KWA MWAKA akiwa na damu aliyoitoa kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za watu wengine (WAEBRANIA 9:6-7).  Vilevile kulikuwa na pazia lililowatenganisha Wayahudi na wale wasio Wayahudi (Mataifa) katika hekalu.  Sasa kwenye saa hii ya kusali nguvu ya ajabu isiyoonekana iliyararua mapazia na kuyafanya vipande Kila mmoja akashikwa butwaa pamoja na makuhani.  Pale msalabani, kwa damu yake Yesu, alitupa kila mmoja wetu uwezo wa kuzungumza na Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa Kuhani, na pia alitoa pazia lililotutenganisha Mataifa na Wayahudi (WAEBRANIA 10:19-20; WAEFESO 2:14-18).

    NCHI IKATETEMEKA  – Tetemeko hili liliwafanya wenye dhambi wote, pamoja na askari waliomlinda kutetemeka kwa hofu.  Dhambi huleta hofu kubwa.  Siyo hilo tu, nchi ilitetemeka kwa hofu na woga wa kufunua kinywa chake kummeza Yesu Kristo ambaye damu yake inanena mema kuliko ya Habili (WAEBRANIA 12:24).  Ikiwa nchi ililaaniwa kwa kumeza damu ya Habili, ni zaidi sana kwa Yesu.  Ilikuwa ni rahisi kufunua kinywa chake na kuwameza Kora, Dathani na Abiramu na watu wa nyumba zao, waliokuwa wamemwasi Mungu (HESABU 16:27-34), kuliko kummeza Yesu asiyekuwa na doa.  Hivyo nchi ilitetemeka.  Vilevile nchi ilitetemeka kwa ajili ya watu wenye dhambi waikaao (AMOSI 8:4-8).

    MIAMBA IKAPASUKA  – Wanadamu wakimpuuza Mungu na kuacha kumsifu Yesu mawe yatapiga kelele.  Hapa yalifanya hivyo.  Siyo hilo tu, hapa Yesu Kristo aliyaendea majeshi ya Shetani kwa ghadhabu na hasira kuu kwenda kuyavua mamlaka.  Hasira na ghadhabu hiyo ilifanya miamba kupasuka na nchi kutetemeka (NAHUMU 1:6; WAAMUZI 5:4; ZABURI 68:7-8).  Vilevile Yesu Kristo ni mwamba, miamba yote hupasuka mbele zake.  Siyo hilo tu kwa imani katika damu ya Yesu, mioyo yetu iliyo migumu kama jiwe au miamba hupasuliwa na kufanywa mioyo laini kama ya nyama (EZEKIELI 36:26-27).  Ndipo tunapoweza kuziona amri zake ni rahisi mno maana tumetakaswa, tumetahiriwa mioyo yetu.

    MAKABURI YAKAFUNUKA  – Makaburi ya Watakatifu waliojulikana Yerusalemu, yalifunuka wakati wa kufa kwa Yesu na kuleta utisho mkuu.  Hata hivyo, walitoka makaburini mwao BAADA YA KUFUFUKA KWAKE YESU kwa kuwa Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, limbuko lao waliolala (1 WAKORINTHO 15:20; UFUNUO 1:5).  Baada ya Yesu kufufuka, watakatifu hawa walifufuka nao na kuwatokea wengi Yerusalemu, Tukimwamini Yesu, kama alivyokwenda mbinguni, sisi nasi tutakwenda huko.  Kama alivyofufuka, sisi nasi tutafufuliwa katika Ufufuo wa Uzima (YOHANA 5:28-29).  Akida, yaani mkuu wa kikosi, na maaskari wenzake walipoyaona haya, NDIPO wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.  Haupaswi kungojea kuyaona haya, ndipo tumkiri Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, au ni Bwana na Mwokozi wa Ulimwengu.  Hatupaswi kungojea haya ndipo tukubali wokovu.  Tutakuwa tumechelewa.  Wakati wa Kunyakuliwa kwa Kanisa kutakakofanyika wakati wowote kuanzia sasa, Watakatifu watatoka makaburini namna hii na wenye dhambi wataogopa na kutetemeka, na kumkiri Yesu wakati wamechelewa.  Watakaochukuliwa ni wale waliookoka pasipo kuona, bali kwa imani (2 WAKORINTHO 5:7).

 

(3)      WANAWAKE KUMTUMIKIA MUNGU    (MST 55-56)

 

Ni uongo wa Shetani kwamba wanawake hawawezi kuwa Watumishi wa Mungu, wakahubiri, wakafundisha, wakatoa pepo au kumtumikia Mungu kwa namna nyinginezo.  Wanawake kumtumikia Mungu, ni jambo la Ki-Biblia hasa.  Nyakati hizi za mwisho, Roho wa Mungu atamwagwa kwa WOTE, binti watatabiri (kuhubiri ni kutabiri pia) na Roho huyu wa Mungu atamwagwa kwa WATUMISHI WA MUNGU WANAUME NA WANAWAKE (MATENDO 2:17-18).  Nyakati za Kanisa la Kwanza, wanaume na wanawake, wote walikuwa watendakazi, wakilihubiri Neno na kulifundisha (MATENDO 8: 1, 4).  Inatupasa kufuata mfumo huu wa ki-Biblia.  Mara kwa mara, katika Biblia, wanawake, wamekuwa na ujasiri wa kumtumikia Mungu na kuwa wanyenyekevu na watii kwa Yesu Kristo na Neno lake, kuliko wanaume.  Hapa tunaona wanawake waliomfuata Yesu kutoka Galilaya, karibu maili 100 kutoka Yerusalemu, wakija kumtumikia Yesu.  Hapa msalabani, hawakuwako wanafunzi wale kumi na moja wa Yesu kasoro Yohana (YOHANA 19: 25-26).  Wengi walikuwa wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea (LUKA 23:27).  Wanawake walikuwepo msalabani mpaka mwisho na tena walikuwapo kwenye mazishi yake (MST 61) na pia wanawake ndiyo waliokuwa wa kwanza kwenda kulitazama kaburi siku ya kufufuka kwa Yesu (MATHAYO 28:1).  Mwanamke ndiye aliyewapelekea habari za kufufuka kwa Yesu, Petro na Yohana, na kuwatia moyo, NDIPO nao wakachangamka!  Hapo mwanzo, walikuwa wamekata tamaa na kwenda kuvua samaki (YOHANA 20:1-3; 21:1-3).  Mwanamke Priska au Prisila alikuwa tayari kukatwa kichwa kwa ajili ya Injili aliyokuwa anaihubiri Paulo na Mwanamke Fibi aliwasaidia wengi mno (WARUMI 16:1-3).  Shime wanawake, tutende kazi ya Bwana! Wanaume pia tupate changamoto kwa watendakazi wanawake ambao wanatenda kazi ya Mungu kwa bidii pamoja na majukumu mengi ya kifamilia waliyo nayo.

 

(4)      KUZIKWA KWA YESU    (MST 57-61)

 

  Baada ya kufa, Yesu alizikwa.  Sisi nasi baada ya kufa pamoja naye inatupasa kuzikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo (WAKOLOSAI 2:12).  Ikiwa tumeifia dhambi kwa kufa pamoja na Kristo kweli, hatuwezi kuwa wabishi kuhusu ubatizo wa maji tele baada ya kuokoka.  MAITI HASEMI, HUZIKWA TU!  Tena kumzika maiti, ni kumfunika kabisa kwa udongo, siyo kumnyunyizia udongo usoni.  Vivyo hivyo, ubatizo ni wa maji tele (YOHANA 3:22-23).  Mwanafunzi wa Yesu aliyekubaliwa kupewa maiti, alikuwa mtu tajiri, mstahiki (Mheshimiwa), mtu wa baraza ya mashauri (MATHAYO 27:57-58; MARKO 15:42-43).  Watu tuliookoka tulio matajiri, wenye vyeo, wenye elimu, inatupasa tuyatumie hayo kwa ajili ya kuishindania Injili.

 

(5)       KULINDA KWA KABURI   (MST 62-66)

 

  Wakuu wa Makuhani walimwita Pilato, BWANA, lakini Yesu walimwita MJANJA (MST 62-63).  Ndivyo walivyo viongozi wengi wa dini leo.  Walililinda kaburi na kulitia muhuri au lakiri ambayo siyo rahisi kuifungua, bila kujulikana, wakafikiri ni salama, lakini Yesu akafufuka.  Hata tukiwazuia watu kuifuata kweli kwa kuwazuia kwa lakiri, wataifuata kweli tu.  Neno la Mungu halifungwi (2 TIMOTHEO 2:9). FULL GOSPEL

No comments: