Je Unafahamu uzuri wa Mbinguni?
Mpendwa msomaji, pole sana na shughuli nyingi za kila
siku. Ninajua kwamba muda wako ni
mchache sana, kutokana na shughuli zako nyingi.
Hata hivyo ninakuomba muda wako mfupi tu, ili tuzungumze juu ya jambo
muhimu ambalo nimeona kwamba ni vema nikushirikishe. Je umekubali ombi langu? Natumaini umekubali. Asante sana.
Basi ninakusihi tufuatane pamoja katika mazungumzo haya.
Mpendwa msomaji, huenda utakuwa umewasikia watu wengi
wanaofiwa na ndugu, jamaa au marafiki zao wapendwa, wakisema, “Mungu waweke
mahali pema peponi“. Jambo hili
linadhihirisha jinsi kila mmoja wetu anavyoamini kwamba kuna mahali pema peponi
yaani mbinguni na tena inaonyesha jinsi sisi sote tunavyopenda kwenda huko,
sisi na jamaa zetu. Je wewe una shauku
ya kwenda mahali pema peponi au mbinguni, baada ya kuiaga dunia hii? Najua wewe pia una shauku ya kwenda mbinguni
siku moja. Hata hivyo, shauku yako
itaongezeka zaidi utakapokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu uzuri wa
mbinguni. Peponi au mbinguni, ni wapi na
kukoje? Peponi au mbinguni, kuna uzuri
usioweza kufananishwa. Tukifahamu jinsi
mbinguni kulivyo kuzuri, kila mmoja wetu atazidi kuwa na shauku ya kufika huko
siku moja. Mpendwa msomaji, tufuatane
basi ili upate ufahamu wa kutosha kuhusu mbinguni au peponi.
Peponi au mbinguni
ni wapi na kukoje?
Mbinguni au peponi, ni juu sana, mbingu ya tatu. Biblia inasema katika 2 WAKORINTHO 12: 2-4,
“Namjua mtu mmoja katika kristo,……Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya
tatu. Nami namjua mtu huyo…….ya kuwa
alinyakuliwa mpaka Peponi………” Mbingu ya
tatu ni wapi? Mbingu ya kwanza, ni hii
iliyo na mawingu yanayoleta mvua, na mawingu mengine. Ni anga hili lililo juu ambalo sehemu yake
huonekana kwa macho ya kawaida. Ndege au
eropleni zote zinazobeba abiria, huruka katika mbingu hii ya kwanza. Mbingu ya pili, ni mbingu iliyo mbali zaidi yenye sayari na
nyota zote. Sayari zilizoko katika mbingu ya pili ni pamoja na Zebaki, Zuhura,
Mars, Mshtarii, Zahali, Uranus, Neptune, na Pluto. Sayari nyingine ziko mbali sana. Kwa mfano umbali wa dunia yetu kutoka kwenye
jua ni maili 93 milioni (kilometa 148,800,000), lakini umbali wa sayari ya
pluto kutoka kwenye jua ni maili 3,666 milioni (Karibu kilometa 5,900
milioni). Nyota ziko nyingi sana,
zinakisiwa kufikia 400 bilioni! Nyota ziko mbali sana na dunia yetu. Nyota iliyo karibu zaidi na dunia, iko karibu
maili 26,000 bilioni (karibu kilometa 42,000 bilioni). Sasa basi, baada ya sayari zote hizi na nyota
hizi, ndiyo tunafika mbingu ya tatu.
Mbingu ya tatu, au mbinguni, au Peponi, kwa msingi huu ni kilometa
mabilioni kwa mabilioni kutoka hapa duniani.
Yesu kristo alipopokelewa na wingu, na kupaa kwenda juu mbinguni
(MATENDO 1:9-11), alikwenda mbali sana kiasi hiki. Huko ndiko waliko watakatifu waliotutangulia.
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
. Mbinguni au peponi, ni kilometa mabilioni kwa
mabilioni kutoka hapa duniani
Tupige hatua tena na kuangalia mambo mengine. Sasa je, mtu anapokufa, anasafirije kwenda
mbinguni, mbali kiasi hiki? Hatupaswi
kuogopa kifo, ikiwa tunaishi maisha yaliyo mbali na dhambi. Biblia inasema katika ZABURI 116:15, ”Ina
thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake”. Kufa kwa watakatifu ni faida (WAFILIPI
1:21). Ni heri kwa wafu wafao katika
Bwana (UFUNUO WA YOHANA 14:13). Kufa kwa
mtu anayeishi maisha yaliyo mbali na dhambi, ni mwanzo tu wa utukufu. Mtu anayeishi maisha mbali na dhambi, anapokufa,
roho yake humiminwa katika mwili mwingine wa roho unaitwa mwili wa mbinguni,
kama mafuta yaliyo katika chombo kibovu kinachovuja, yanavyoweza kumiminwa
katika chombo kingine kilicho kizuri.
Kufa ni kumiminwa! Mtume Paulo
aliyepata neema ya kuchukuliwa na kupelekwa mpaka mbingu ya tatu wakati wa uhai
wake (2 WAKORINTHO 12:2-4), ulipofika wakati wa kufariki kwake, alijua ni
wakati mzuri wa kumiminwa. Kwa maneno
yake, katika 2 TIMOTHEO 4:6, alisema, “Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na
wakati wa kufariki kwangu umefika”.
Kuhusu miili ya mbinguni, Biblia inasema katika 1 WAKORINTHO
15:40-41, 44, “Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani, lakini fahari
yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine
ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota……Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia
uko”. Miili hii tuliyo nayo ni mibaya
sana. Ni kama vyombo vibovu. Fahari
yake, yaani uzuri wa ile miili ya mbinguni ni zaidi sana kuliko miili hii tuliyo
nayo. Miili ya mbinguni inang`aa mno na
kupendeza sana. Mtu huwa na mwili mzuri
zaidi ya ule wa malaika! Mtakatifu anapokata roho, roho yake mara moja
humiminwa katika mwili mzuri wa jinsi hii.
Mtu akiwa katika mwili wa mbinguni, atapenda kujitazama wakati
wote. Mwili huu hauna makovu wala ulema
wala hauna makunyanzi ya uzee! Baada ya
mtu kuwa na mwili mzuri wa jinsi hii, huvikwa mavazi mazuri meupe sana
yanayometameta sana. Weupe wa mavazi
haya, ni weupe usio na mfano duniani (UFUNUO WA YOHANA 3:4-5; UFUNUO WA YOHANA 7:9; MARKO 9:2-3). Baada ya kuvikwa mavazi haya, mtu
hufunguliwa mlango wa gari na malaika, na kuingizwa katika gari zuri sana
lisilokuwa na mfano duniani. Yako mabilioni ya magari ya Mungu, yanayowasubiri
watakatifu. Biblia inasema katika ZABURI
68:17, “Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu”. Mtu huchukuliwa na malaika katika magari haya
yanayoitwa magari ya moto, yanayoambatana na farasi wa moto na kuchukuliwa
kwenda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli (LUKA 16:22; 2 WAFALME 2:11).
Mtu hufunguliwa mlango wa gari na malaika, na kuingizwa
katika gari zuri sana
lisilokuwa na mfano duniani
Magari yanayoitwa magari ya kifahari yanayowabeba Marais na
Wafalme duniani kama Mercedes Benz, BMW n.k; si mali kitu yanapolinganishwa na
magari haya. Magari ya Mungu hayatumii
dizeli au petroli, bali huendeshwa na upepo wa kisulisuli, na huenda kasi sana. Kwa muda mfupi sana, mtu hufika mbinguni, na
hulakiwa na malaika waliotanda njiani kushoto na kulia wakiimba nyimbo za
shangwe, inayopita ile ambayo huwako mbinguni, mtu mmoja anapotubu dhambi zake
hapa duniani (LUKA 15:10, 32). Hakuna
mapokezi yoyote ya Rais au Mfalme yeyote duniani, yanayolingana na mapokezi ya
mtu anayeingia mbinguni, yanayofanywa na malaika.
Sasa tupige hatua nyingine.
Mbinguni kwenyewe kukoje?
Mbinguni ni nchi iliyo bora kuliko nchi yoyote duniani (WAEBRANIA
11:16). Waza juu ya nchi yoyote duniani
inayowavutia watalii wengi kutokana na uzuri wake. Nchi hii siyo mali kitu ikilinganishwa na
Peponi. Mbinguni ni kuzuri mno! Hakuna
usiku wala mchana. Hakuna joto wala
baridi. Jua au mwezi havitumiki kutoa
mwangaza. Utukufu wa Mungu ndiyo nuru ya mbinguni (UFUNUO WA YOHANA
21:23-25). Neno “Peponi”, linatokana na
neno la kiyunani, “Paradeisos”, linalotafsiriwa pia, “Paradiso”, na kwa tafsiri
fasaha, lina maana, “bustani nzuri kubwa iliyojaa matunda mazuri” na tena lina
maana “mahali palipojaa furaha na raha kuu isiyo na kifani” (UFUNUO WA YOHANA
2:7; WAEBRANIA 4:1, 11). Matunda ya miti iliyomo katika bustani hii
isiyokuwa na mfano, ni pamoja na mti wa uzima uzaao matunda aina kumi na mbili.
Maisha mbinguni, ni pamoja na kula matunda haya katika bustani ya Mungu, na kupunga
upepo wa raha kuu isiyo kifani, Paradiso (UFUNUO WA YOHANA 2:7; UFUNUO WA YOHANA 22:2).
Kipi cha ziada tena kuhusiana na mbinguni? Mbinguni ni mji uliobuniwa na kujengwa na
Mungu (WAEBRANIA 11:10, 16). Miji yote
ya dunia hii imebuniwa na kujengwa na wanadamu wenye upungufu wa ubunifu wa
michoro, fedha, vifaa n.k; Mbinguni, ni
mji uliobuniwa na Mbunifu Mkuu, Mungu mwenyewe mwenye uwezo wote. Hakuna mji kama huu duniani. Barabara zake siyo za lami, bali ni za
dhahabu iliyo kama kioo kiangavu ambayo hakuna mfano wake duniani. Mtu anapotembea barabarani, hujiona kama
katika kioo (UFUNUO WA YOHANA 21:21).
Katika YOHANA 14:2, Yesu anasema katika mji huu kuna “makao” mengi. Neno la Kiyunani linalotafsiriwa hapa “makao”
ni “mone”, linalotafsiriwa katika kiingereza “Mansion”, katika Biblia ya
tafsiri ya King James Version. “Mansion”
ni jumba kubwa la kifahari. Jumba la
Meya wa Jiji la London, Uingereza (Lord Mayor of London), linaitwa “Mansion
House”. Vinyo hivyo mbinguni, kuna makao mengi, au majumba mengi ya
kifahari. Kila mtu atakayeingia
mbinguni, atapewa “kao” au “jumba mojawapo la kifahari”, la kuishi. Kao lako linakusubiri! Majumba haya,
hayakujengwa kwa tofali za sementi au udongo, bali kuta zake zimejengwa kwa
madini ya aina nyingi. Biblia inasema katika UFUNUO WA YOHANA 21:18-20, “Na
majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi
mfano wa kioo safi. Na misingi ya ukuta
wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili
yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita
akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda (tisa) yakuti ya
manjano; wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili
amethisto”.
Vito hivi au madini haya, yanafanya majumba ya mbinguni,
yapendeze mno. Yaspi, ni madini
yanayong’ara sana yenye rangi ya kijani iliyochanganyika na bluu. Yakuti samawi, ni mawe ya bluu, mazuri sana
yenye ugumu unaofuatia madini ya almasi.
Kalkedoni, ni aina ya madini mazuri sana yenye rangi aina nne mbalimbali
– nyekundu iliyochanganyika na njano, hudhurungi (brown) iliyochanganyika na
nyeusi, bluu iliyochanganyika na nyeupe, na rangi ya maziwa. Zumaridi, ni madini yenye rangi ya damu.
Krisolitho, ni madini yaliyo kama dhahabu, ila yana rangi ya kijani
iliyochanganyika na njano. Zabarajadi, ni madini maangavu (yanayoona ndani),
yenye rangi ya bluu iliyochanganyika na kijani. Yakuti maanjano, ni madini
mazuri yenye rangi ya njano na mchanganyiko wa kijani. Krisopraso, ni madini yenye rangi tatu
pamoja; njano, kijani na bluu.
Hiakintho, ni madini yenye rangi nyekundu iliyochanganyika na
njano. Amethisto, ni madini yenye rangi
ya zambarau, yenye bluu na wekundu ndani yake.
Nini zaidi? Mwangaza
wa mbinguni siyo kama wa duniani usio na rangi.
Mwangaza wa mbinguni ni wa rangi ya yaspi yaani kijani iliyochanganyika na bluu (UFUNUO
21:11). Mavazi meupe ya wale walioko
mbinguni, hubadilika rangi mara kwa mara kutokana na rangi ya mwangaza na ya
majengo hivyo kufanya watu wapendeze mno.
Ndani ya makao ya mbinguni kuna fenicha za kifahari. Fenicha alizoagizwa Musa kuzitengeneza na
kuziweka katika maskani, zilikuwa mfano tu wa fenicha za mbinguni (WAEBRANIA
8:5; KUTOKA 25:9-40). Chemichemi za maji na mito ya maji ya uzima
inauzunguka mji. Mbinguni kuna kula na kunywa, hakuna mauti wala maumivu au
taabu (LUKA 22:14-16, 29-30; UFUNUO WA
YOHANA 2:17; UFUNUO WA YOHANA 21:4-5; UFUNUO WA YOHANA 14:13). Kuna kuimba nyimbo za sifa, na vinanda
(UFUNUO WA YOHANA 14:2-3; UFUNUO WA
YOHANA 15:2-4). Ufahamu wetu utaongezeka (1 WAKORINTHO 13:12). Kuna mengi zaidi yasiyotamkika katika lugha
hii ya duniani (2 WAKORINTHO 12:4). Ni
heri twenda wenyewe kujionea. Tusikubali
mume au mke kutuzuia kuingia mbinguni maana mbinguni hakuna kuoa au kuolewa
(LUKA 20:34-36; MATHAYO 22:30).
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho
kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).
Kinyonge ni kipi? Ni yule
anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa,
ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha
kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia
mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA
14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili
upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati
kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa
ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge,
mwenye dhambi. Sistahili kuingia
mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu
Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la
Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia
mbinguni. Ili uzidi kudumu katika
utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho
katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU
AKUBARIKI !!!
FULL GOSPEL
No comments:
Post a Comment