HAZINA ILIYOSITIRIKA NA MFANYABIASHARA
(MATHAYO 13:44-46)
Katika mistari hii Yesu anatufundisha juu ya Ufalme wa
mbinguni kwa kutumia mifano miwili.
Hazina iliyositirika, na mfanyabiashara mwenye kutafuta lulu nzuri. Kuna mengi ya kujifunza katika mifano hii
tunapoichambua mmoja baada ya mwingine.
(1)
HAZINA ILIYOSITIRIKA (MST. 44)
Katika mfano huu, HAZINA ni Taifa la Israeli (ZABURI 135:4;
MALAKI 3:17). MTU anayeitafuta hazina
hii ni Yesu Kristo mwenyewe (LUKA 19:10; MATHAYO 15:24; MATHAYO 10:6). Hazina hii imesitirika au imefichika katika
SHAMBA. Shamba hili ni Ulimwengu
(MATHAYO 13:38). Yesu alipokuja kwa Waisraeli,
hawakumpokea, WALIJIFICHA (YOHANA 1:11; MATHAYO 23:37-39; WARUMI 10:16,
19-21). Baada ya Yesu kuiona hazina
iliyositirika katika shamba, yaani kuwaona Waisraeli wamejificha kwa kukataa
kumpokea, alilinunua shamba lote, yaani ulimwengu wote. Kwa damu yake iliyomwagika msalabani,
aliununua ulimwengu wote na siyo taifa la Israeli tu (YOHANA 11:49—52; MATHAYO
21:43; 1 WAKORINTHO 6:19-20; MATENDO
20:28; 2 PETRO 2:1; WARUMI 11:11-12).
Hazina hii ingawa Yesu ameiona, bado imefichika mpaka wakati Yesu
atakapokuja mara ya pili duniani na wakati huo hazina ya Mungu, Waisraeli wote,
watakaokuwa hai wakati huo; wataokoka (WARUMI 11:25-32).
MAMBO YA ZIADA YA KUJIFUNZA KATIKA MFANO HUU
Mambo mengi ya
Ufalme wa Mungu ambayo ni hazina, yamesitirika, ni mafumbo. Yako chini sana ya ardhi. Hayako juujuu tu. Inabidi kuchimba sana chini kwa maombi,
kusoma na kujifunza Neno, kujitenga na ulimwengu n.k.; na kuyatafuta kwa bidii
ili kuyapata
(LUKA 6:48; DANIELI 2:22; 1
WAKORINTHO 2:10).
Tukitaka kuwa
Watumishi wa Mungu wakubwa kwa kumletea hazina kubwa Yesu Kristo katika uvuvi
wetu wa watu, ni lazima tufahamu kwamba samaki wengi wakubwa baharini
hawapatikani ufukoni tu, wanapatikana kilindini, chini sana ya bahari. Ni lazima tuwe tayari kwenda kilindini kwa
maombi na kujitoa kwetu katika muda, fedha, na kuhubiri kwa wakati unaofaa na
usiofaa, tukizidi kupanda neno ndani ya watu (LUKA 5:4-7). Tupande Neno ndani ya watu asubuhi na jioni
kila siku, hatimaye mavuno mengi ni dhahiri (MHUBIRI 11:6).
Injili imesitirika
au imefichwa kwa watu ambao hawajaokoka.
Inabidi mtu afunuliwe ili alielewe Neno la Mungu (2 WAKORINTHO
4:3-4; MATHAYO
11:25-27). Ni juu yetu kuchimba chini
sana kwa maombi ili watu waijue kweli.
2. MFANYABIASHARA MWENYE KUTAFUTA
LULU NZURI (MST. 45-46)
LULU, ni aina fulani ya madini ya thamani kubwa ambayo
hupatikana katika wanyama fulani wa baharini wenye gamba au kombe wa aina ya
chaza (oyster). Lulu hizi hupatikana
kutoka kwa wanyama hawa wanapopatwa na aina fulani ya maradhi yanayosadikika
kuchukua miaka saba. Kama lulu hizo
hazipatikani katika kipindi hicho wanyama hao hufa, na lulu zikapotea. Thamani ya lulu moja, ni karibu US $ 400,000,
ambazo ni karibu TShs. 200,000,000.
Kuingia mbinguni ni kama kupata lulu nzuri yenye thamani kubwa kuliko
hata maisha yetu hapa duniani (MATENDO 20:24).
Imani halisi ya wokovu, ni ya thamani kama lulu (2 PETRO 1:1). Ahadi ya Yesu aliyosema amekwenda kutuandalia
makao, ili pale alipo sisi nasi tupate kuwapo (YOHANA 14:1-3); ni ya thamani
sana kwetu kama lulu
( 2 PETRO 1:4). Watu wanaangamizwa
kwa kukosa na kuyakataa maarifa (HOSEA 4:6).
Maarifa ya Neno la Mungu ni ya thamani kama lulu (MITHALI 20:15). Maarifa haya ndiyo ambayo hatimaye
yatatufanya tuuone mji wa mbinguni Yerusalemu mpya uliojengwa kwa lulu (UFUNUO
21:21). Tunapaswa kuwa kama mfanya
biashara mwenye kutafuta lulu hii – imani hii na maarifa haya na tukiipata,
tuuze vyote tulivyo navyo na kuinunua.
Mfanyabiashara ana sifa saba zifuatazo:
Hutangatanga
kutafuta mali. Tuwe tayari kutangatanga
na kuwa tayari kuliacha kanisa lisilofundisha kweli. Hilo silo lulu. Mfanyabiashara haendelei na biashara isiyompa
faida kwa sababu ya kuizoea tu!
Huwa tayari
kufuata mali hata kama iko mbali.
Tusiridhike tu kusali kwenye makanisa ya karibu. Tuweke mtaji mkubwa, tuwe tayari kutoa nauli
kubwa kufuata Kanisa linalotupa maarifa kama Malkia wa Kusini (MATHAYO 12:42);
Huwa tayari kutoa
muda wote, nguvu zake zote na hata kupata mateso na dhiki ili apate mali. Tufanye vivyo hivyo ili tuupate ufalme wa
mbinguni.
Hujikana nafsi
yake, hujinyima hata usingizi na anasa za ulimwengu ili apate mali na
asifilisike. Sisi nasi tujikane nafsi
zetu ili tuupate ufalme wa mbinguni (LUKA 9:23-25);
Huwa tayari
kuwaacha ndugu, mke, wazazi, marafiki na kwenda mbali kusiko na ndugu na kukaa
huko miaka mingi kutafuta mali. Vivyo
hivyo tunapaswa kuwa tayari kuacha vyote ili kuupata ufalme wa mbinguni (LUKA
14:25-26, 33);
Huwa na watu
wanaomjia kumshawishi ili amalize fedha zake kama malaya n.k; na pia huwa macho
kujilinda na wezi wanaopanga kumwibia mali zake. Sisi nasi tukeshe na kuomba ili kujilinda na
wezi na malaya wanaotaka kuiba lulu zetu.
Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji (lulu) yako;
Haridhiki au
hatosheki na fedha hata kama anazo kiasi gani.
Tunapaswa kujiona hatuna kitu wakati wote (WAGALATIA 6:3) na kujiona
kwamba hatujafika wala hatujawa wakamilifu (WAFILIPI 3:12-15). Tudumu kuwa tayari kujifunza Neno la Mungu
wakati wote. Tusitosheke na viwango vya
Utakatifu na utendaji kazi tulivyo navyo mpaka tufikie kimo na cheo cha
utimilifu wa Kristo (WAEFESO 4:15).
Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam (MATHAYO 13:51).
Ikiwa umeyafahamu, PIGA VITA VIZURI VYA IMANI, ILINDE IMANI
YA WOKOVU KAMA LULU. TUONANE PARADISO
KWENYE
Usikose faida zilizomo katika somo”PUNJE YA HARADALI NA
CHACHU” katika link
hiihttps://davidcarol719.wordpress.com/punje-ya-haradali-na-chachu/
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho
kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).
Kinyonge ni kipi? Ni yule
anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa,
ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha
kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia
mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA
14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili
upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati
kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa
ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge,
mwenye dhambi. Sistahili kuingia
mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu
Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”.
Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku
ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa
linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!! FULL GOSPEL
No comments:
Post a Comment