AGIZO LA KUTAWADHANA
Leo, katika Siku hii ya Kuichambua Biblia, tunaendelea tena
kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.
Leo tunajifunza na kutafakari kwa makini YOHANA 12:37-50 na YOHANA
13:1-5. Katika mistari hii, pamoja na
mambo mengine, tutajifunza juu ya “AGIZO LA KUTAWADHANA“. Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika
mistari hii, katika vipengele vinane:-
(1) UWEZEKANO WA KUTOKUSADIKI BAADA YA KUONA MIUJIZA
(12:37-41);
(2) ALAMA KUU YA KUKISUJUDIA NA KUJIABUDU KIUMBE BADALA YA
MUNGU (12:42-43);
(3) MAHUBIRI YA MWISHO KWA WAYAHUDI WASIOAMINI (12:44-50);
(4) UPENDO WA YESU KWA WATU WAKE (13:1);
(5) UWEZEKANO WA SHETANI KUTUTIA MOYO WA KUMSALITI YETU
(13:2);
(6) YESU ALITOKA KWA MUNGU (13:3);
(7) NIFANYALO WEWE HUJUI SASA LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE
(13:7);
(8) AGIZO LA KUTAWADHANA (13:4-15).
(1) UWEZEKANO WA KUTOKUSADIKI BAADA YA KUONA
MIUJIZA (12:37-41)
Yesu Kristo, alifanya ishara au miujiza mikubwa kwa
Wayahudi, lakini hata hivyo, wengi hawakumwamini kwamba yeye ndiye Masihi. Wayahudi waliwaza toka mioyoni mwao kwamba
Neno jema haliwezi kutoka Nazareti (YOHANA 1:46) na tena kutoka Galilaya jimbo
alilotokea Yesu, hakuwezi kutokea nabii (YOHANA 7:47-52). Hawakutaka kabisa kukbadili msimamo wao
huo. Lolote waliloliona au kulisikia kwa
Yesu, walilipima kwa msimamo wao huo. Hata
miujiza aliyoifanya Yesu, waliipima kwa mtazamo au msimamo wao huo, na kuona
kwamba anafanya miujiza na kutoa pepo kwa Beelzebuli mkuu wa pepo (MATHAYO
12:24). Kutokana na kuendelea na mtazamo
wao huo Mungu hakuwafunulia lolote bali aliwapofusha macho na kuifanya mioyo
yao mizito ili wasiongoke au kubadilishwa na kuponywa, na Isaya aliyaona hayo
mapema katika utabiri wake. Hata leo ni
vivyo hivyo. Tukiwa hatuko tayari kubadili
msimamo au mtazamo wetu juu ya Kanisa fulani, mafundisho fulani, hata tuone
Mhubiri wa Kanisa hilo anatumiwa namna gani, hatuwezi kuamini. Hatari yake ni kwamba Mungu hawezi
kutufunulia lolote kwa sababu hatuko tayari kubadili mtazamo wetu. Hatuna budi kuwa na utayari wa kubadili
mitazamo yetu tunaposhuhudiwa vilivyo na Roho Mtakatifu, hata kama
tutadharaulika kwa kufanya hivyo.
Tukifanya hivyo tuna heri.
(2 ALAMA KUU YA
KUKISUJUDIA NA KUKIABUDU KIUMBE BADALA YA
MUUMBA (12:42-43)
Kupenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu, maana
yake, kukisujudia na kukiabudu kiumbe badala ya Muumba (WARUMI 1:25). Tukiwa tumeifahamu Kweli ya Neno la Mungu,
halafu tukaibadili kweli hiyo kuwa uongo, kwa kuogopa kutengwa na masinagogi au
madhehebu yetu, viongozi wetu wa dini, waume zetu, wazazi na ndugu zetu n.k.,
kwa kufanya hivyo, tunakuwa tunawasujudia na kuwaabudu viumbe badala ya
Muumba. Wengi wetu tunafanya hivi pasipo
kujua. Tutaifahamu Kweli fulani kwa
mfano Ubatizo wa Maji tele baada ya kuokoka n.k., lakini tukiona kuitekeleza
kweli hiyo kutatufanya tutengwe na masinagogi au makanisa yetu, waume zetu
n.k., tunachagua kuibadili kweli hiyo kuwa uongo, na hivyo kumwabudu kiumbe
badala ya Muumba. Hatupaswi kufanya hivyo.
(3) MAHUBIRI YA
MWISHO KWA WAYAHUDI WASIOAMINI (12:44-45)
Katika mistari hii tunaona mahubiri ya mwisho ya Yesu, kwa
Wayahudi wasioamini. Baada ya mahubiri
haya, Yesu alihusika katika kuwafundisha na kuzungumza na wanafunzi wake
tu. Katika mahubiri haya, Yesu anazidi
kusisitiza kwamba asiyemwamini Yesu anakaa GIZANI maana Yeye ndiye Nuru ya
ulimwengu. Asiyekubali maneno yake Yesu,
Neno lake ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.
Maagizo ya Mungu, ni uzima wa milele kwetu. Tukipuuza agizo lolote la Mungu na kusema
tutakwenda mbinguni tutakuwa tunajidanganya.
(4) UPENDO WA
YESU KWA WATU WAKE (13:1)
Saa ya Yesu kusalitiwa na kusulibishwa, ilikuwa
imefika. Baada ya mahubiri yake mwisho
kwa Wayahudi wasioamini, alibaki tu na wanafunzi wake. Wanafunzi wake hapa ndiyo wanaoitwa WATU WAKE
YESU. Anatupenda upeo! Atawaacha wengine kando na kubaki na
sisi! Anajishughulisha sana na mambo
yetu kama mama au baba anavyojishughulisha na watoto wake ambao ndiyo watu wake
(1 PETRO 5:6-7; ZABURI 103:13).
(5) UWEZEKANO WA
SHETANI KUTIA MOYO WA KUMSALITI YESU
(13:2)
Shetani wakati wote hutafuta mtu wa kummeza (1 PETRO
5:8). Haogopi kumjaribu mtu yeyote, awe
ni Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji, Mwalimu, Mama Mchungaji, Kiongozi wa
Zoni, Seksheni, Kiongozi wa Kanisa la Nyumbani au mtu yeyote. Shetani alikuwa na ujasiri wa kumjaribu Yesu
nyikani na kumtaka eti amsujudie! Hapa
tunaona akimtia moyo wa kumsaliti Yesu aliyekuwa Mtume Yuda. Baadaye kidogo Mtume Petro naye aliyesema
ijapompasa kufa hawezi kumkana Yesu, yeye naye alimkana mara tatu (MATHAYO
26:31-35, 69-75). Hatupaswi kujivuna na
kujisahau, na kujiona kwamba sisi hatuwezi kuanguka katika uasherati, uzinzi au
dhambi yoyote na kuacha wokovu.
Tunaweza! Tunalotakiwa kufanya,
ni KUJILINDA na KUKESHA na KUOMBA tukiitumainia neema ya Mungu wakati wote (1
YOHANA 5:18; MATHAYO 26:41). Kujilinda
ni kuwa mbali na mtego wowote unaotunyemelea wa kutufanya tufanye uasherati au
uzinzi au dhambi yoyote.
(6) YESU ALITOKA
KWA MUNGU (13:3)
Yesu hakuanzia tumboni kwa Bikira Mariamu kama wengine
wanavyofikiri. Alitoka kwa Mungu. Alikuwa ni Mungu aliyedhihirishwa kwetu katika
mwili ( 1 TIMOTHEO 3:16). Bikira Mariamu
alikuwa ni mama yake Yesu katika mwili.
Yesu alitoka kwa Mungu, ni Mungu, kisha akarudi mbinguni. Hivyo Bikira Mariamu siyo mama yake
Mungu. Yeye mwenyewe anajiita majakazi
(mtumwa wa kike) wa Bwana (LUKA 1:38).
Jua linapochomoza, siyo kwamba halikuwako kabla, ila lilikuwa
linaonekana kwa wengine katika nchi nyingine.
Yesu, JUA LA HAKI; alipozaliwa na Mariamu, alikuwa NURU (Jua) iliyochomoza
vivyo hivyo.
(7) NIFANYALO
WEWE HUJUI SASA LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE (13:7)
Kiongozi wetu, hupewa mafunuo ya mambo yajayo kala yetu
tunaoongozwa, ili aweze kutuongoza katika njia vizuri. Kwa msingi huu, wakati mwingine Kiongozi wetu
wa Kanisa anaweza akatuambia tufanye mambo ambayo hatujayafahamu vizuri matokeo
yake, maana yake n.k, Hatuna budi
kufanya mara moja na kutoka, bila kujua tuendako kama Ibrahimu (WAEBRANIA
11:8). Hatimaye ndipo tutakapofahamu
vizuri maana ya yale tuliyoambiwa kuyafanya na Kiongozi wetu aliyepewa mafunuo
kabla yetu sisi.
(8) AGIZO LA
KUTAWADHANA (13:4-15)
Hapa tunaona Yesu akiwatawadha miguu wanafunzi wake na
kutupa agizo la kutawadhana miguu sisi kwa sisi (13:14). Watu wengine kwa kutumia maandiko haya,
huleta makarai ya maji makanisani mwao na kutaka watu watawadhane miguu. Hivi sivyo tunavyoaagizwa kufanya. Hatuoni popote katika Kanisa la Kwanza
wakifanya hivyo katika vitabuv yote vinavyofuata hadi Ufunuo wa Yohana. Sasa agizo hili maana yake nini? Nyakati za Biblia watu hawakuwa na viatu vya
kuingiza kama vyetu, hivyo walipotembea, walijaa vumbi katika miguu na ilibidi
kuosha miguu yao, au kutawadha, kabla ya kuingia ndani ya nyumba (WIMBO ULIO
BORA 5:3; MWANZO 24:31-32; 43:24; WAAMUZI 19:17-21; 2 SAMWELI 11:8; 1 TIMOTHEO
5:10). Ilivyokuwa desturi, ni kwamba,
wakati wote mtumwa au aliyekuwa mdogo ndiye aliyemtawadha mkubwa au Bwana wake
(MWANZO 18:1-4; 19:2; 1 SAMWELI 25:41).
Sasa hapa Yesu aliye Mkubwa, Bwana na Mwalimu, anawatawadha wadogo
(wanafunzi wake), lilikuwa fumbo. Ndiyo
maana Petro alikataa mwanzoni, na Yesu akawauliza hatimaye, “Je! Mmeelewa na
haya niliyowatendea?“ (13:12). Hapo
mwanzo aliwafundisha kwa nadharia juu ya unyenyekevu, na mkubwa kuwa mdogo,
waliposhindania ukubwa, lakini hawakuelewa (LUKA 22:24-27; MATHAYO
20:20-28). Sasa hapa kwa KITENDO
(Practical) anawafundisha kwa kielelezo.
Yeye aliye mkubwa anachukua nafasi ya mtumwa, mdogo. Hili ndilo agizo lake kwetu kunyenyekeana
sisi kwa sisi, na kufuta kushindania au kutafuta ukubwa. Petro aliyekuwepo hapa, baada ya hapa
hatufundishi kutawadhana miguu kwa maji, bali anatufundisha unyenyekevu (1
PETRO 5:5). Mtume Paulo naye anasisitiza
hilo (MATENDO 20:19; WAFILIPI 2:5-7).
Kwa msingi huu, Petro, alipokemewa na Paulo aliyekuja nyuma yake
(mdogo), aliyenyenyekea tu (WAGALATIA 2:7-10).
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho
kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).
Kinyonge ni kipi? Ni yule
anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa,
ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha
kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia
mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema
hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati
kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa
ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge,
mwenye dhambi. Sistahili kuingia
mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la
Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia
mbinguni. Ili uzidi kudumu katika
utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho
katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU
AKUBARIKI !!! (FULL GOSPEL)
No comments:
Post a Comment