HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU
Leo, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA na tutaangalia
kwa makini YOHANA 1:15-28. Katika
mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya, “HAKUNA MTU
ALIYEMWONA MUNGU”. Tutayagawa mafundisho
tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vitano:-
(1)WAJIBU WA KUMSHUHUDIA YESU (Mst. 15);
(2)YESU NI ZAIDI YA NABII (Mst. 15);
(3)NEEMA NA KWELI (Mst. 16-17);
(4)HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU (Mst. 18);
(5)KUJITAMBULISHA KWA YOHANA MBATIZAJI (Mst. 19-28).
(1) WAJIBU WA
KUMSHUHUDIA YESU (Mst. 15)
Yohana alimshuhudia Yesu, akapaza sauti yake. Kila mtu aliyeokoka ni shahidi wa Mungu
(ISAYA 43:10). Mara tu baada ya
kuokolewa, kila mmoja wetu anawajibika kumshuhudia Yesu kwa watu wote kwamba ni
Mwokozi mwenye uwezo wa kumsamehe mtu dhambi zake na kumpa uwezo wa
kuzishinda. Tunapaswa kushuhudia hivi
waziwazi kwa kumkiri Yesu mbele ya watu, tukipaza sauti zetu bila aibu kama
Yohana. Tukiionea haya Injili yaani
kumwonea haya Yesu na kuacha kumshuhudia, yeye naye atatuonea haya na kuacha
kutukubali kuingia mbinguni (WARUMI 1:15-16; LUKA 9:26; MATHAYO 10:32-33). Vile vile tunajifunza hapa kwamba katika
kushuhudia kwetu tunapaswa kumshuhudia Yesu anayeokoa. Hatupaswi kushuhudia kwamba dini zetu au
madhehebu yetu ndiyo mazuri kuliko mengine.
Tuwashuhudie watu juu ya Yesu Mwokozi, wakiisha kuokolewa, ndipo
tuwaeleze kuja kujifunza Neno la Mungu Kanisani ili waukulie Wokovu (1 PETRO
2:12; 1 YOHANA 1:1-2).
(2) YESU NI ZAIDI
YA NABII (Mst. 15)
Yesu alikuja nyuma ya Yohana Mbatizaji, lakini amekuwa mbele
yake, kwa maana alikuwa kabla yake!
Maana yake nini maneno haya? Yesu
kama mtu au mwanadamu alizaliwa na tena kuanza huduma yake nyuma ya Yohana
Mbatizaji. Alikuja ulimwenguni nyuma ya
Yohana Mbatizaji. Yohana alimtangulia
kuzaliwa na kuanza huduma. Hata hivyo,
Yesu kama Mungu, alikuwako kabla ya Yohana Mbatizaji (YOHANA 8:58; WAKOLOSAI
1:17-18; MIKA 5:2). Yesu amekuwa mbele
yake Yohana maana yake yeye ni mkuu zaidi kuliko Yohana Mbatizaji (YOHANA 1:27;
3:30-31). Yesu anaitwa mkuu, Mwana wa
Aliye juu (LUKA 1:31-32), lakini Yohana Mbatizaji anaitwa Nabii wake aliye juu
(LUKA 1:76). Yesu ni zaidi ya nabii. Yesu ni Mungu pamoja nasi (MAHAYO 1:23;
WAFILIPI 2:5-8). Kwa misingi hiihii,
Bikira Mariamu ni mama yake Yesu kama mwanadamu, lakini siyo mama yake Yesu
kama Mungu. Mungu hana mama (WAEBRANIA
7:3). Kuna jambo jingine la kujifunza
hapa. Yohana Mbatizaji alimtangulia Yesu
kuzaliwa na kuanza huduma ya Utumishi wa Mungu hapa duniani, lakini alipokuja
Yesu nyuma yake, huduma yake ilikuwa kuu kuliko ya Yohana. Hatupaswi kuona ajabu. Mungu anaweza kufanya huduma ya mtu
aliyezaliwa nyuma, kuokoka nyuma na kuanza huduma nyuma ya wazee
waliomtangulia, kuwa na huduma iliyo kuu kuliko ya wazee hao. Mungu anaweza kumbariki mdogo, akamwacha
mkubwa kama kwa Yakobo na Esau au kwa Efraimu na Manase (WARUMI 9:10-16; MWANZO
48:8-19).
(3) NEEMA NA
KWELI (Mst. 16-17)
Neno Neema lina maana mbili.
Neema, ni upendeleo wa kuchaguliwa, bila kustahili kutokana na matendo
yoyote aliyoyafanya mtu au sifa aliyo nayo mtu.
Neema pia, ni uwezo wa kushinda katika tabia na Utumishi wa Mungu
sawasawa na mapenzi yake, tunaopewa na Mungu bila gharama yoyote au nguvu zetu. Tunaokolewa kwa neema tu kwa njia ya imani
(WAEFESO 2:4-5, 8-9). Baada ya kuokoka
pia, ni muhimu kufahamu kwamba tunafanya mapenzi yote ya Mungu kwa Neema ya
Mungu. Tumepokea Neema juu ya Neema. Torati ilikuja kwa mkono wa Musa. Yesu aliileta kweli. Kweli ya Yesu ni ngumu zaidi kuifanya kuliko
Torati (MATHAYO 5:27-28; 38-41; 43-48).
Hata hivyo siyo sisi tunaofanya.
Tukijifunza juu ya kweli yoyote na kuona ni ngumu, hatuna haja ya
kuikimbia bali tunatakiwa kukikaribia kiti cha neema cha Mungu kwa ujasiri na
hapo tunapoomba neema tunapewa neema ya kutuwezesha kuyafanya
tuliyojifunza. Kwa neema hiyo, Yesu
ndiye anayefanya ndani yetu lile linalompendeza Mungu (WAEBRANIA
13:20-21). Torati ya Musa haikuwa na
msaada wowote wa kumsaidia mtu kuifanya.
Hakika tumepokea NEEMA JUU YA NEEMA, NEEMA NA KWELI!
(4) HAKUNA MTU
ALIYEMWONA MUNGU (Mst. 18)
Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote maana yake
nini? Mbona maandiko mengine yanataja
watu waliomwomba Mungu? (ANGALIA KUTOKA
24:9-11). Linalosemwa hapa ni kwamba mtu
hawezi kumwona Mungu kwa MACHO YA KIMWILI.
Yako macho ya aina nyingi. Yako
macho haya yanayoonekana na tena yako macho tunayoyatumia kuona katika ndoto
wakati macho haya ya kawaida tumeyafumba, na tena yako macho ya rohoni. Mtu hawezi kumwona Mungu ambaye ni Roho kwa
MACHO YA KIMWILI, akaishi, kwa macho ya kimwili, mtu anaweza kumwona Mungu kwa
sehemu tu ya umbo na siyo uso (HESABU 12:8; KUTOKA 33:17-23; 1 TIMOTHEO
6:16). Hata hivyo, mtu anaweza kumwona
Mungu anapokuwa katika Roho, kwa macho ya rohoni. Mahali popote mtu alipomwona Mungu, alimwona
katika hali hii, macho ya mwili na mwili wote ukiwa hauna sehemu katika jambo
hili (UFUNUO 1:9-10; 2 WAKORINTHO 12:1-4; EZEKIELI 1:1, 26-28; DANIELI 7:9;
MATENDO 7:56). Katika roho, mtu ndipo pia
anaweza kusema na Mungu uso kwa uso kama rafiki yake (KUTOKA 33:11). Tunalojifunza hapa ni kwamba, Musa na watu
wengine waliomwona Mungu kwa macho ya rohoni, walifanya hivyo kwa muda kidogo
tu na wakarudia macho ya mwilini, lakini Yesu ambaye ni Mungu Mwana ndiye pekee
aliye karibu na Baba (kifuani pake), hivyo wakati wote amekuwa akimwona. Huyu ndiye aliyemfunua Mungu kwetu. Tukiiona tabia ya Yesu alipokuwa duniani,
tumeiona tabia ya Mungu. Ni chapa ya
nafsi yake (YOHANA 14:8-9; WAEBRANIA 1:3).
Yesu ni zaidi ya Musa! Huyu ndiye
aliyemfunua Mungu kwetu kuliko Musa maana anamjua zaidi. Katika nyumba ya Mungu, Musa anaitwa
mtumishi, na Yesu anaitwa mwana (WAEBRANIA 3:5-6). Mtumishi wa nyumbani hawezi kumfahamu Baba
mwenye nyumba kama mwana wake mwenyewe! Inatupasa kumsikia Yesu zaidi kuliko
Musa (MATHAYO 17:1-5).
(5)
KUJITAMBULISHA KWA YOHANA MBATIZAJI (Mst. 19-28)
Wayahudi walituma kwake makuhani na walawi (wasaidizi wa
makuhani) kutoka Yerusalemu na wakamwuliza Yohana Mbatizaji, “WEWE U NANI?”
(Mst.19). Makuhani walikuwa watu wasomi wa neno la Mungu, wenye mamlaka katika
Uyahudi na watu walioheshimiwa sana.
Hawa kutokana na kusoma kwao, walitarajiwa zaidi kumfahamu Yohana
Mbatizaji ni nani kuliko watu wengine, lakini hawakuwa wamefunuliwa. Mara kwa mara Waheshimiwa, Wasomi na watu
wenye mamlaka katika jamii ambao tunatarajia wangekuwa wanaelewa upesi kuhusu
wokovu, hawa wamekuwa hawapati mafunuo yoyote kutokana na kiburi na majivuno
yao. Kwa kukosa mafunuo, wamekuwa wakiuliza “Wokovu ni nini? Yesu ni nani?
Kweli ni nini?” n.k. (YOHANA 18:37-38; MATHAYO 11:25). Kutokea kwa Yohana Mbatizaji kulikuwa kwa
kushangaza miongoni mwa Wayahudi. Baada
ya maisha yake ya utoto, hawakumwona kabisa tena. Maisha yake yalikuwa majangwani akila nzige
na asali ya mwitu mpaka alipotokea kwao (LUKA 1:80; MATHAYO 3:4). Mara tu baada ya kutokea na kuanza kuhubiri,
makuhani walishangaa kuona watu wote wanamwendea na kubatizwa na kushangaa
kwamba mbona anabatiza? (MATHAYO 3:1-2,
5-8; YOHANA 1:25). Mtu hawezi kuwa
Mtumishi wa Mungu anayetumiwa na Mungu mpaka awe tayari kuishi mbali na watu
muda mwingi wa maisha yake na kutenga muda mrefu akizungumza na Mungu kuliko
watu. Mtu anayependa mazungumzo na watu
wakati wote, hawezi kutumiwa na Mungu kuvuta maelfu ya watu kama Yohana
Mbatizaji. Wachungaji wanaopenda
mazungumzo na mizaha na kukaa kwenye magenge ya watu wa kawaida, watashangaa
sana huduma ya mtu anayeishi majangwani jinsi inavyovuta watu wengi na kuuliza
HUYU NI NANI? MBONA HATUMJUI! Wanaweza
wakafikiri anatumia hirizi au uganga kuwabatiza wengi hivyo! Yohana Mbatizaji hakutumia hirizi au uganga,
siri ilikuwa kukaa majangwani.
Alijitambulisha kwamba yeye ni sauti ya mtu aliaye nyikani.
JE, UNATAKA KUOKOKA SASA?
Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake
wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.
Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa
hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja.
Je, kweli utasamehewa? Jibu ni
Ndiyo! Yesu mwenyewe anasema katika
YOHANA 6:37, “……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”. Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii,
utasamehewa na kupata wokovu. Je, uko
tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na
kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi? Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya
toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda
dhambi. Je, uko tayari kuifuatisha sala
hii sasa? Najua uko tayari. Basi sema maneno haya, “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa
kumaanisha kuziacha. Naomba unisamehe na
kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani. Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa. Liandike sasa jina langu katika kitabu cha
uzima mbinguni. Asante kwa kuniokoa,
katika Jina la Yesu, Amen”. Sasa
ninaomba kwa ajili yako, “Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote,
na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka
zote katika Jina la Yesu, Amen”. Tayari
umeokoka. Ili uzidi kuukulia wokovu,
hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI!!!
No comments:
Post a Comment