CHUKI NA MAUDHI KWA MKRISTO
Mkristo, ni mtu anayemfuata Yesu Kristo katika tabia, na
utumishi wake kwa Mungu. Mkristo, ni mtu
aliyezaliwa mara ya pili, mtu aliyeokoka.
Watu ambao hawajaokoka, siyo Wakristo kwa msingi wa Biblia. Katika somo la leo la Kuichambua Biblia, tutatafakari
kwa makini YOHANA 15:18-27; 16:1-4.
Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine kadha, tunajifunza kipekee
juu ya “CHUKI NA MAUDHI KWA MKRISTO“.
Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii katika
vipengele kumi na viwili:-
(1) MAANA YA
“ULIMWENGU“ (15:18);
(2) ULIMWENGU
HUWAPENDA WALIO WAKE (15:19);
(3) ULIMWENGU
HUWACHUKIA WATU WASIO WA ULIMWENGU (15:19);
(4) ULIMWENGU
HUWACHUKIA NA KUWAUDHI WATUMISHI WA MUNGU
(15:19-20);
(5) MTUMWA SI
MKUBWA KULIKO BWANA WAKE (15:20);
(6) ULIMWENGU
KUTOKULISHIKA NENO (15:20);
(7) SABABU YA
ULIMWENGU KUTUCHUKIA NA KUTUUDHI (15:21; 16:3);
(8) WAJIBU WA
KUONDOA UDHURU WA WENYE DHAMBI (15:22);
(9) WALINICHUKIA
BURE (15:23-26);
(10) ROHO
MTAKATIFU HUMSHUHUDIA YESU PAMOJA NASI (15:26-27);
(11) SABABU YA
KUELEZWA MAPEMA JUU YA KUCHUKIWA NA
KUUDHIWA (16:1,4);
(12) KUTENGWA
HATA KUUAWA KWA WAKRISTO (16:2)
(1) MAANA
YA “ULIMWENGU“ (15:18)
Ni muhimu kufahamu maana ya neno “Ulimwengu“, kabla ya
kuendelea kujifunza somo hili. Neno
“Ulimwengu“, kama linavyotumika katika mistari hii, linamaanisha watu wa
Ibilisi yule mwovu, watu ambao hawajaokoka; pamoja na mkuu wa ulimwengu Ibilisi
mwenyewe. “Ulimwengu“, pia unawajumuisha
watu wanaojiita wameokoka, wakati bado ni watu wanaoipenda dunia na marafiki wa
dunia, yaani wanafanya mambo yote tu kama mataifa (1 YOHANA 5:18-19; YOHANA
14:30; YAKOBO 4:4; 1 YOHANA 2:15-17).
Watu waliookoka wanaoishi maisha yaliyo tofauti na ulimwengu, hawa si wa
ulimwengu huu (YOHANA 17:14,16).
(2)
ULIMWENGU HUWAPENDA WALIO WAKE (15:19)
Watu wanaonena ya dunia, husikiwa na dunia na kupendwa na
ulimwengu (1 YOHANA 4:5; YOHANA 7:7).
Shetani, pamoja na watu ambao hawajaokoka, na pia watu wanaojiita
wameokoka lakini wanfanya mabo yote kama mataifa, huwapenda wanaofanana nao,
watu wa ulimwengu. Watu wanaofanya
dhambi na kuipenda dunia, hupendwa na ulimwengu, kwa sababu hawana tofauti
nao. Tukidai kwamba tumeokoka, huku
ulimwengu unatupenda, madai yetu si ya kweli.
(3)
ULIMWENGU HUWACHUKIA WATU WASIO WA ULIMWENGU (15:19)
Ulimwengu, huhukumiwa sana unapowaona watu wanaoishi maisha
ya utakatifu; kwa sababu hiyo huwachukia.
Shetani, mkuu wa ulimwengu, hujawa wivu mwingi anapowaona watu wanaoishi
maisha ya utakatifu, kwa sababu anajua kwamba hawa wanakwenda mbinguni, mahali
asipoweza kuingia, na hivyo huwachukia.
Kwetu Wakristo, hatuapswi kustaajabu, tukiona ulimwengu unatuchukia (1
YOHANA 3:13). Ikiwa tunaushuhudia
ulimwengu ya kuwa kazi zake ni mbovu, ulimwengu lazima utuchukie na
kutuudhi. Tangu mwanzo, Mungu aliweka
uadui kati ya nyoka (shetani) na mwanamke pamoja na uzao wake (MWANZO
3:14-15). Warithi wa mbingu, siku zote
ni maadui wa watu wa ulimwengu huu. Watu
wasio haki huwachukia wenye haki sikuzote.
Kaini kwa msingi huu alimchukia habili mwenye haki; akamwua. Baba yetu wa mbinguni akitupenda kwa kuwa
tunazishika amri zake wale tunaokaa nao dunia wenye dhambi, hutuchukia. Kwa msingi huu, Yusufu alichukiwa na nduguze
(MWANZO 37:3-4). Sauli alipooona na
kutambua ya kwamba Bwana alikuwa pamoja na Daudi, Sauli akawa adui yake Daudi
SIKU ZOTE ( 1 SAMWELI 18:28-29). Ndivyo
ilivyo hata leo, Bwana akiwa pamoja nasi, ulimwengu huwa adui kwetu (WAGALATIA
4:28-29).
(4)
ULIMWENGU HUWACHUKIA NA KUWAUDHI WATUMISHI WA MUNGU
(15:19-20)
Watumishi wa
Mungu wanaohubiri kweli ya Neno la Mungu na kussshuhudia
ulimwengu ya kuwa kazi zake ni mbovvvu, ulimwengu
huwachukia. Mfalme Ahabu,
mtu wa ulimwengu, kwa msingi huu, alimchukia Nabii Mikaya
mwana wa Imla
aliyehubiri kweli (YOHANA 7:7; 2 NYAKATI 18:6-7). Watu vuguvugu wanaojiita
wameokoka, huku wanaipenda dunia, kwa jinsi hiihii, kama
Ahabu huwachukia
Watumishi wa Mungu wanaoihubiri kweli. Hatupaswi kuona ajabu.
(5) MTUMWA
SI MKUBWA KULIKO BWANA WAKE 15:20
Watu tuliookolewa, ni watumwa wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunapokuwa Watumishi wa Mungu, tunapaswa
kufahamu kwamba mafanikio yetu katika huduma zetu, hayana budi kufuata misingi
aliyoitumia Yesu hata kupata mafanikio.
Yesu aliomba hata kulia sana na machozi (WAEBRANIA 5:7). Sisi, siyo wakubwa kuliko Yeye, hivyo
tusitazamie mafanikio bila maombi. Yesu
alikuwa mchapakazi (YOHANA 9:4), sisi nasi hatuna budi kuwa wachapakazi au siyo
hatuwezi kufanikiwa. Siyo hayo tu. Yesu aliudhiwa na kudhihakiwa. Aliambiwa amerukwa na akili, ana pepo tena ni
Msamaria yaani mtu asiye na Mungu (MARKO 3:21; YOHANA 8:48). Nasi tutaudhiwa vivyo hivyo.
(6)
ULIMWENGU KUTOKULISHIKA NENO (15:20)
Ikiwa watu wa ulimwengu walilipuuza Neno lake Yesu mwenyewe,
sembuse neno letu tutakalolihubiri na kuwafundisha? Hatupaswi kuona ajabu tukiwahubiria
walimwengu, wengine wakakata shauri na wengine wakatutukana. Ynapotupata haya tuendelee tu kuhubiri kama
Mtume Paulo (MATENDO 19:8-10; 28:23-24, 30-31).
(7) SABABU
YA ULIMWENGU KUTUCHUKIA NA KUTUUDHI (15:21; 16:3)
Sababu kuu ya ulimwengu kutuchukia na kutuudhi baada ya
kuokoka na kuishi maisha ya utakatifu, ni kwa kuwa hawamjui Mungu Baba wala
hawamjui Yesu (1 YOHANA 2:3-4). Tukiwa
tumeokoka na kukaa katika mapenzi ya Mungu, waume zetu, wazazi wetu, marafiki
zetu wa zamani, Boss wetu kazini, wote hawa watatuchukia ikiwa wao hawajaokoka,
kwa sababu hawamjui Yesu. Tunapaswa
kuwasamehe tu na kusonga mebele. Kamwe
tusiache wokovu kwa sababu ya maudhi haya.
Kuna baraka au heri tele tukifanya hivi ( 1 PETRO 4:12-16).
(8) WAJIBU
WA KUONDOA UDHURU WA WENYE DHAMBI (15:22)
Pamoja na maudhi na dhihaka za wenye dhambi, kila mtu
aliyeokoka anawajibika KUSEMA NAO, na kuwahubiria juu ya wokovu. Wakikataa kuacha dhambi, hawana udhuru siku
ya mwisho.
(9)
WALINICHUKIA BURE (15:23-25)
Yesu alitnda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, hata hivyo
walimchukia. Wao wenyewe walisema,
“Namna hii hatujapata kuiona kamwe“.
Aliponya vilema, vipofu, na viziwei wao, hata hivyo, walimchukia
bure. Hayo pia yatatupata sisi. Tunaweza tukawafanyia yote mema waume zetu au
wazazi wetu ambao hawajaokoka, lakini bado watatuchukia. Hatupaswi kuonaajabu. Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake. Vivyo hivyo, leo, mtu yeyote anayemchukia
Yesu na kukataa kuokoka, wakati aliteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zetu,
kufanya hivyo, ni kumchukia bure. Kwa
nini tufanye hivyo? Kumchukia Yesu, ni
kutafuta madhara makubwa siku ya hukumu.
(10)
ROHO MTAKATIFU HUMSHUHUDIA YESU PAMOJA NASI (15:26-27)
Faida kubwa ya kujazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ni kuwa na
Msaidizi anayemshuhudia Yesu pamoja nasi.
Mtu aliyejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, anapokuwa anahubiri, Roho
Mtakatifu huhubiri pamoja naye, na hivyo matokeo yake kuwa makubwa, na rahisi,
maana huyo Roho humhakikishia mtu tunayemhubiri kwamba ni mwenye dhambi na
tunayosema ni haki na ni kweli na kwamba kuna hukumu inayomsubiri (YOHANA
16:7-8). Sisi hatuwezi kufanya
hayo. Yeye atanishuhudia, nanyi pia
mnashuhdia!
(11)
SABABU YA KUELEZWA MAPEMA JUU YA KUCHUKIWA NA
KUUDHIWA
(16:1,4)
“Nimewaambia, msije mkachukizwa, nimewaambia haya, ili
makusudi saa ile
itakapokuja mayakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia“. Makusudi ya Yesu
kutueleza mapema kwamba tutachukiwa na kuudhiwa, ni ili
yatakapotokea tusione
ni mageni, na tena tushinde na kusonga mbele. Hapa pia tunajifunza wajibu wa
Mwalimu wa Biblia.
Inatupasa kufundisha masomo ya kinga kwa Wakristo,
tukiwafundisha mapema mambo ambayo watayasikia au kukutana
nayo.
Wakikutana na mafundisho potofu baada ya sisi kuwafundisha
mapema kwa Biblia,
ni vigumu kwao kupotezwa.
(12)
KUTENGWA HATA KUUAWA KWA WAKRISTO (16:2)
Watu waliookolewa walitengwa na masinagogi yao baada ya
KUPIGWA (MATHAYO 10:17). Hapa Yesu
anasema hiyo haitoshi. Watatuua
wakidhani ni thawabu kwao. Ndivyo ilivyo
leo kwa watu wanaosema Yesu siyo Mwana wa Mungu. Wakimwua Mkristo kwa jambia, wanadhani ni
thawabu, wanadhani wamemtolea Mungu ibada.
Pamoja na haya yote, hatupaswi kubabaika (WARUMI 8:35-39). FULL GOSPEL
No comments:
Post a Comment