CHAKULA CHA YESU KRISTO
Leo tena, tunazidi kusonga mbele katika kujifunza Kitabu cha
YOHANA katika Biblia zetu. Leo,
tunajifunza YOHANA 4:27-45. Pamoja na
mafundisho mengine tutakayojifunza katika mistari hii, tutajifunza pia juu ya
“CHAKULA CHA YESU KRISTO“. Tutayagawa
mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinane:-
(1)UHUSIANO WA WANAUME NA WANAWAKE KATIKA WOKOVU (Mst. 27);
(2)WAJIBU WA KUUACHA MTUNGI (Mst. 28-30);
(3)CHAKULA CHA YESU KRISTO (Mst. 31-35);
(4)MSHAHARA WA KUMTUMIKIA MUNGU (Mst. 37-38);
(5)MMOJA HUPANDA AKAVUNA MWINGINE (Mst. 37-38);
(6)NENO LA MWANAMKE (Mst. 39);
(7)WALIMSIHI AKAE KWAO (Mst. 40-42);
(8)NABII HAPATI HESHIMA KATIKA NCHI YAKE (Mst. 43-45).
(1) UHUSIANO WA
WANAUME NA WANAWAKE KATIKA WOKOVU (Mst. 27)
Yesu Kristo, aliangalia sana uhusiano wake na wanawake
kwamba hauleti dosari yoyote katika usafi wake na ushuhuda wa wokovu wa Injili
yake. Alipokuwa akisema na mwanamke
Msamaria pale kisimani, wanafunzi wake walistaajabu kwa sababu alikuwa akisema
na mwanamke. Siyo kwamba Yesu alikuwa
hasemi na wanawake kabisa, la hasha!
Alisema nao (LUKA 10:41; 23:28-31; 8:47-48; YOHANA 20:16-17). Katika tukio la kisimani, wanafunzi wake
walishangaa kumwona Yesu akiwa na mwanamke yule Msamaria peke yao. Hawakuwahi kuona hivyo kabla. Lakini hata hapa, utaona kwamba ilikuwa ni
hadharani – kisimani, mahali ambapo watu wanaingia na kutoka na kuyasikia yote
waziwazi. Ndiyo maana “hakuna aliyesema,
Mbona unasema naye?“ Wakati wote, katika
lolote, Yesu Kristo alikuwa mwangalifu katika lolote alilolifanya na
wanawake. Aliangalia kwa makini na
kuhakikisha kwamba hakuna yeyote atakayesema “Wokovu ni uongo au Injili
anayohubiri siyo ya kweli“. Mtume Paulo
vivyo hivyo, alipokuwa anakwenda nyumbani kwa mwanamke Lidia, hakuwa peke yake,
alikuwa na wenzake Timotheo na Sila.
Katika timu walifanya kazi miongoni mwa wanawake. Maneno “Tukaenda“, “Tukaketi“, “Tukasema“,
“Akatusihi“, “Ingieni“, yanaonyesha kwamba walikuwa wengi (MATENDO 15:40-41,
16:1-2, 13-15). Katika utendaji wake wa
kazi, pale Paulo Mtume alipokuwa peke yake, alimchukua Akila na Prisila mkewe,
wakaenda kutenda kazi na kuwa huru kuingia katika nyumba yoyote au kusema na
yeyote. Mtume Paulo, hakwenda na
mwanamke Prisila katika Injili bila kuwa na mumewe. Sisi nasi hatuwezi kufanya hivyo. Hakuna kielelezo chochote cha wokovu wetu
tunaohubiri, ikiwa mwanaume atakuwa anatembea barabarani au kuzunguka huko na
huko, na mwanamke ambaye siye mke wake, kwa kisingizio cha kuitenda kazi ya
Bwana (MATENDO 18:1-4). Baada ya kuokolewa,
tunapaswa kuhakikisha SIKU ZOTE kwamba tunakuwa na dhamiri isiyo na hatia. SIYO MBELE ZA MUNGU TU, ILA NA MBELE ZA
WANADAMU, ili mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia
yaani WOKOVU (MATENDO 24:16; 2 WAKORINTHO 8:20-21). Watu ambao hawajaokoka wakimwona mwanaume
aliyeokoka anatembea barabarani huku na huko na mwanamke ambaye siye mke wake
au wako chumbani peke yao kwa visingizio vya kujifunza Biblia na kuomba;
watasema wanafanya uasherati, hata kama siyo kweli. Tayari hiyo ni hatia. Uasherati haupaswi kutajwa kwetu kamwe hata
kwa kudhaniwa (WAEFESO 5:3). Mataifa
wakiona wokovu siyo kweli kutokana na uhusiano wetu na wanawake, tendo hilo ni
kuwawekea vikwazo vya kuwazauia kuingia mbinguni, wakati sisi wenyewe hatuingii
(MATHAYO 23:13; LUKA 11:52; ISAYA 57:14; WALAWI 19:14; 1 YOHANA 2:10). Kutembeleana kwa “kaka“ na “dada“ katika
wokovu kwa visingizio vya kutembeleana katika ugonjwa n.k; vinaweza kuleta
zinaa katika wokovu (2 SAMWELI 13:6-15).
Mwanaume atamshika mwanamke asiye mke wake mkono tu, katika salamu; siyo
mabega, nywele au sehemu yoyote nyingine.
Wanawake watawafuatilia wanawake na vivyo hivyo wanaume. Hakuna “boyfriend“ au “girlfriend“ katika
wokovu. Hata wachumba ni mwiko
kutembeleana na kupikiana vyumbani mpaka baada ya ndoa. Hata kuja kanisani mwanaume hapaswi
kuzungumza na mwanamke mambo yasiyopasa kwa mfano “Binti mbona nyinyi wanawake
mnatukataa wanaume kila tunapowachagua muwe wake zetu?“ Huo ni uasherati.
(2) WAJIBU WA
KUUACHA MTUNGI (Mst. 28-30)
Tukitaka kumpendeza Mungu, ni lazima tuwe tayari kuiacha
mitungi yetu na kwenda kufanya kazi ya Mungu.
Mtungi ni chochote kinachoonekana ni cha muhimu kwetu duniani. Ni lazima tuache biashara zetu na kwenda
Kanisani au kufuatilia watoto wachangas kiroho.
Lolote lile iwe watoto, mume, kazi ya Kaisari n.k; yote hayo ni
mitungi. Tusiruhusu yatuzuie kumtumika
Mungu. Mwanamke huyu alipoacha mtungi
wake, aliwaleta wengi kwa Yesu.
Asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wa Yesu (LUKA
14:3).
(3) CHAKULA CHA
YESU KRISTO (Mst. 31-35)
Chakula kwa mwanadamu, ni kitu ambacho tunakitolea muda wetu
wote. Katika kufanya kazi tunatafuta
chakula, tunatumia saa nyingi kwa siku katika kula asubuhi, mchana na
usiku. Bila chakula cha mchana, wengine
wataona maisha magumu mno. Chakula cha
Yesu Kristo kilikuwa kuyatenda mapenzi ya Mungu yaani kuihubiri Injili ili watu
waokoke kama kwa mwanamke huyu Msamaria.
Hicho ndicho kilichokuwa chakula Na. 1, kwa Yesu. Chakula cha mwili kilifuata baadaye. Sisi nasi inatupasa kumfuata kwa kutoa maisha
yetu yote kuihubiri Injili na kuwasimamisha watoto wachanga katika wokovu
(YOHANA 13:15; 1 PETRO 2:21).
(4) MSHAHARA WA
KUMTUMIKIA MUNGU (Mst. 36)
Mshahara mkubwa unamsubiri kila mtu anayetoa muda wake mrefu
kumtumikia Mungu. Wengi kwa kutokuelewa,
wanafikiri kumtumikia Mungu ni kazi isiyo na faida. Inaweza ikaonekana hivyo hapa duniani, lakini
kama tungepata ufahamu, kila mmoja wetu angetafuta kwa bidii, kumtumikia Mungu,
kwa gharama yoyote; ili ajilimbikizie mshahara tele wa milele mbinguni (ISAYA
49:4; 2 NYAKATI 15:7; 1 WAKORINTHO 15:58).
(5) MMOJA HUPANDA
AKAVUNA MWINGINE (Mst. 37-38)
Kabla ya wanafunzi wa Yesu, manabii wengi walikufa kwa ajili
ya Neno la Mungu. Yohana Mbatizaji pia
alikatwa kichwa kwa ajili ya Injili na wengi wengine. Yesu naye ilimpasa kufa kwa misingi
hiyohiyo. Hata baadaye mitume nao
walikufa vivyo hivyo, pamoja na wamishonari wengi. Wote hawa wamepanda, nasi tunavuna hivi
leo. Tunaweza kumhubiri mtu
asiokoke. Tumepanda mbegu kwa kufanya
hivyo atakuja kuvuna mwingine. Yote ni
sawa, tuzidi kuitenda kazi (1 WAKORINTHO 3:6-8; MHUBIRI 11:4-6).
(6) NENO LA
MWANAMKE (Mst. 39)
Neno la Mwanamke Msamaria siku ileile aliyokuwa ameokoka,
lilileta watu wengi kwa Yesu. Wanawake
hatupaswi kujidharau. Mungu huwatumia wanawake kipekee kuwaleta wengi kwa Yesu,
pale tu wanapoondoa kujidharau na kujiamini.
Wako manabii wengi waliokuwa wanawake katika Biblia – Miriamu (KUTOKA
15:20), Hulda (2 WAFALME 22:14), Noadia (NEHEMIA 6:14), Debora (WAAMUZI 4:4),
Anna (LUKA 2:36). Shime tuitende kazi ay
Bwana. Siyo kwa uwezo wetu, bali kwa
uwezo wa Mungu tunaitenda kazi (ZEKARIA 4:6; WARUMI 9:16).
(7) WALIMSIHI
AKAE KWAO (Mst. 40-42)
Walipomsihi Yesu akae kwao zaidi, uamsho uliendelea. Sisi nasi inatupasa kuendelea kumsihi Yesu na
Roho Mtakatifu kwa maombi kila siku, ili uamsho uendelee kati yetu, ikiwa
wanakaa kwetu.
(8) NABII HAPATI
HESHIMA KATIKA NCHI YAKE (Mst. 43-45)
Yesu Kristo, hakupokelewa vema na kupata heshima, Nazareti,
hapo alipolelewa (LUKA 4:16, 22-30; MATHAYO 13:54-55). Sisi nasi itakuwa hivyo. Tunaweza tukawashuhudia ndugu zetu wasikubali
ushuhuda wetu. Ikiwa hivyo, tuwaunganishe
na wale wasiowajua.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho
kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).
Kinyonge ni kipi? Ni yule
anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa,
ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha
kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia
mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA
14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili
upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati
kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa
ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge,
mwenye dhambi. Sistahili kuingia
mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu
Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la
Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia
mbinguni. Ili uzidi kudumu katika
utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho
katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU
AKUBARIKI !!! ( FULL GOSPEL)
No comments:
Post a Comment